emblem

Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim

Habari

DKT. SALIM AHMED SALIM ATAJWA KUIMARISHA MSINGI WA DIPLOMASIA YA TANZANIA


Katika Kongamano la kwanza la maazimisho ya kumuenzi Dkt.Salim Ahmed Salim imeelezwa kuwa, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu Balozi Dkt. Salim Ahmed Salim amekuwa msingi na chachu ya maboresho makubwa yaliyofanyika kwenye sera ya mambo nje nchini, na kwamba kupitia yeye Tanzania imetengeneza msingi imara wa wigo wa kidiplomasia Duniani

Hayo yamezungumzwa leo, Jumanne Septemba 30.2025 na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Dkt. Salim Ahmed Salim, lililoandaliwa na Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (Chuo cha Diplomasia), lililofanyika kwenye ukumbi wa Kilimanjaro, Makao makuu ya CRDB Bank, jijini Dar es Salaam

Mtoa mada mkuu wa kongamano hilo, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba amemtaja Balozi Dkt. Salim Ahmed Salim kuwa ni mzalendo wa kweli kwa Taifa lake, na kwamba katika uongozi wake alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha anaifahamu vyema Tanzania na matatizo ya Watanzania ili kuyatafutia majawabu

Katika maelezo yake Jaji Warioba amesema sifa iliyonayo Tanzania kwenye jumuiya ya kimataifa inaenda sambamba na msingi mkubwa uliowekwa na Mwanadiplomasia huyo mbobevu aliyejizolea sifa sio tu hapa nchini, bali Afrika na Duniani kwa ujumla wake

Balozi (mstf) Modest Jonathan Mero aliyewahi kuiwakilisha Tanzania Umoja wa Mataifa (New York, Vienna, Geneva), ambaye alikuwa mtoa mada wa pili kwenye kongamano hilo amesema Umoja wa Mataifa (UN) unamtambua Balozi Dkt. Salim Ahmed Salim kama mtetezi wa maslahi ya nchi nyingine pale inapobidi licha ya kwamba alikuwa anaiwakilisha Tanzania

Naye, Deus Kibamba, Mhadhiri wa Kituo hicho na mtoa mada wa tatu kwenye kongamano hilo amemdadavua Balozi Dkt. Salim Ahmed Salim kwa kumtaja kuwa mstari wa mbele kitaaluma hasa kujikita kwake kwenye utafiti, uchambuzi na uchapishaji uliomuongoza vyema katika utekelezaji wa majukumu yake kama mwakilishi wa Tanzania kwenye jumuiya ya kimataifa

Awali akimkaribisha mgeni rasmi kutoa hotuba yake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Balozi Ramadhan Mwinyi amesema kituo hicho kina mipango kabambe ya kuhakikisha kinamuenzi kwa vitendo Dkt. Salim Ahmed Salim, na kwamba kwa sasa tayari kimeanzisha ushirikiano na Balozi mbalimbali lengo likiwa ni kuifungua Tanzania kiuchumi na kidiplomasia

Kongamano hilo limeenda kwa kauli mbiu isemayo: 'Daraja la Kimataifa, Sauti za Afrika: Kadhimisha Urithi wa kudumu wa Dkt. Salim Ahmed Salim'