Habari
USHIRIKIANO WA KIDIPLOMASIA ULIOPO KATI YA TANZANIA NA CHINA UNAZIDI KUIMARIKA
Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Jamhuri ya Watu wa China, Profesa Hao Ping amesema ushirikiano uliopo kati ya China na Tanzania ni wa muda mrefu na unazidi kuimarika katika nyanja ya kidiplomasia.
Mheshimiwa Profesa Ping amesema haya leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Dkt. Felix Wandwe, ndc Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim.
Akizungumza kuhusu mashirikiano yaliyopo baina ya Tanzania na China, Profesa Ping amesema, Tanzania na China zina ushirikiano na urafiki wa muda mrefu na ziara hii ya kimkakati imelenga kuzidi kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili.
“Wakati wa kilele cha jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) lililofanyika hivi karibuni Beijing China, Viongozi Wakuu wa nchi hizi Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliweka mikakati ya kuzidi kuimarisha ushirikiano uliopo. Kupitia ziara hii, tumekitembelea Kituo ambacho ni Taasisi muhimu ya Serikali kuona namna ya kuzidi kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na Taasisi za Kidiplomasia zilizopo nchini China” amesema Profesa Ping.
Kwa upande wake, Dkt. Felix Wandwe ndc akizungumzia historia ya Kituo amesema, Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt Salim Ahmed Salim, awali kilitambulika kama Chuo cha Diplomasia na kilianzishwa mwaka 1978 kwa makubaliano ya nchi mbili za Tanzania na Msumbiji. Lengo kuu la kuanzishwa kwa Chuo hiki lilikuwa ni kutoa mafunzo ya diplomasia na mahusiano ya kimataifa kwa manufaa ya Serikali za nchi hizi mbili na wananchi wake. Alifafanua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 30 Septemba 2023 alibadili jina la Chuo cha Diplomasia na kuwa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kwa kutambua mchango uliotolewa na mwanadiplomasia huyu kwa nchi yake Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla.
Akizungumzia majukumu ya Kituo amesema Kituo kina majukumu ya kutoa mafunzo, kinafanya utafiti na kutoa huduma ya ushauri elekezi katika masuala ya diplomasia, uhusiano wa kimataifa, stratejia, na usuluhishi wa migogoro na ujenzi wa amani. Kituo kinatoa mafunzo ya lugha za kigeni za Kichina, Kifaransa, Kireno, Kispaniola,Kiarabu, Kikorea, Kiingereza na Kiswahili kwa wageni.
Dkt. Wandwe, ndc. amesema China na Tanzania kupitia ushirikiano wa muda mrefu uliopo tangu miaka ya 1960 kuna maendeleo yamefikiwa kupitia miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na reli ya TAZARA, uwanja wa mpira, elimu na uwanja wa ndege wa Zanzibar. Kaimu Mkurugenzi wa Kituo, Dkt. Wandwe ndc amehitimisha kwa kumshukuru Profesa Ping na ujumbe wake kwa kukitembelea Kituo.