Habari
BALOZI MBAROUK: KASI YA MKANDARASI MRADI WA MADARASA HAIRIDHISHI
BALOZI MBAROUK: KASI YA MKANDARASI MRADI WA MADARASA HAIRIDHISHI
Serikali imesema hairidhishwi na kasi ya mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa vyumba tisa vya mihadhara katika majengo ya ghorofa tatu na kazi za nje katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim jijini Dar es Salaam unaogharimu Shilingi Bilioni Nne.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Mbarouk Mbarouk jana alipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi huo uliofikia asilimia 28 ambapo amemtaka mkandarasi Corporation Sole Works Superitendent kukamilisha mradi huo kwa mujibu wa mkataba.
"Serikali kupitia uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza majukumu yake ,imekusudia kufanya maboresho ya miundombinu ya Kituo cha Dkt. Salim Ahmed Salimu kuwa cha kisasa na kimataifa ",alisema Naibu Waziri Mbarouk.
Aliongeza kusema , uongozi wa Kituo hicho unatakiwa pia kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi huo ili mkandarasi akamilishe ndani ya kipindi cha miezi kumi na mbili ya mkataba kuwezesha wanachuo wapate mazingira mazuri ya kujifunzia.
Taarifa zinaonesha kuwa mkandarasi huyo tayari amelipwa Shilingi 838,535,851 kati ya Shilingi 4,450,359,568 ambapo ametakiwa kuongeza spidi ya kazi.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri huyo aliongeza kusema Wizara itaendelea kufanya maboresho ya kimkakati kuwezesha Kituo hicho kutekeleza majukumu yake hatua itakayosaidia kukuza uchumi kupitia Diplomasia.
Mwisho.
