Habari
TUMIENI ELIMU NA MAARIFA MLIYOYAPATA KUTATUA CHANGAMOTO ZILIZOPO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) amesema vijana wanapaswa kutumia elimu na maarifa wanayoyapata baada ya kuhitimu masomo yao kutatua changamoto zinazolikabili taifa pamoja na maisha yao binafsi.
Waziri Kombo amesema haya wakati wa Mahafali ya 28 ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam ambapo jumla ya wahitimu 900 wametunukiwa vyeti katika ngazi na viwango mbalimbali vya elimu.
“Nawapongeza sana kwa kufikia hatua hii muhimu katika maisha yenu, nawasihi na kuwahimiza muitumie elimu mliyoipata kutatua changamoto zinazolikabili Taifa pamoja na maisha yenu ninyi binafsi. Ni muhimu kwenu kutambua kuwa kwa sasa kuna changamoto katika soko, hivyo nawashauri mtumie ujuzi na maarifa mliyoyapata kwa kujiajiri. Tumieni elimu mliyonayo na vipaji vyenu mlivyojaliwa na Mwenyezi Mungu kwa kufanya kazi kwa bidii, juhudi, uadilifu na uaminifu mkubwa, huku mkiweka mbele uzalendo na maslahi ya Taifa letu. Jiwekeeni malengo makubwa yatakayowapa uwezo wa kuwa waajiri wa watanzania wengine waliopo maeneo mbalimbali”, amesema.
Akizungumza kuhusu fursa zilizopo, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeelekeza kila Halmashauri itenge bajeti kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na makundi maalumu kwa shughuli za ujasiriamali ili kukabiliana na tatizo la ajira. “Nawasihi kuchangamikia fursa hizo. Pia kwa wale mliopo kazini nawasihi kutumia elimu mliyoipata kwa kuwa wabunifu na kutatua changamoto za wananchi kupitia kazi zenu” amesisitiza mheshimiwa Balozi Kombo.
Kwa upande wa mabadiliko ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) yanayoendelea kufanyika, ameuelekeza Uongozi wa Kituo kutumia taarifa ya Kamati iliyoundwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kufanya Tathmini ya Ufanisi na Utendaji wa Wizara hususani kwenye eneo la Kituo, na taarifa ya Kamati iliyoundwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inayohusu mapitio ya utendaji kazi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim ili uweze kutoa mapendekezo ya Sheria ya kuanzishwa kwa Kituo na kuandaa Miongozo mbalimbali ikiwemo Muundo wa Uendeshaji.
Mheshimiwa Balozi Kombo, pamoja na maelekezo haya ameuagiza pia Uongozi wa Kituo kutumia fursa hii kuboresha progamu zilizopo ili zikidhi mahitaji ya Wizara, Nchi na Watanzania kwa ujumla wake. Vilevile, ameagiza zifanyike tafiti zenye kutoa majibu ya changamoto zilizopo katika nyanja ya kitaifa, kikanda na kimataifa ili kuweza kuishauri Serikali ipasavyo.
“Sambamba na hilo, ongezeni jitihada za kuanzisha mashirikiano na taasisi nyingine za kidiplomasia hasa zile zilizo nje ya nchi”, amesema.
Mheshimiwa Waziri Mahmoud Thabit Kombo (Mb), ameuagiza uongozi wa Kituo kuhakikisha unashirikiana na Wizara kuandaa namna bora ya kutoa elimu kuhusu Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la mwaka 2024). “Nitoe rai kwa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuandaa utaratibu rasmi ili Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kitumike kwa ajili ya kutoa elimu ya Sera hii kwa wizara, taasisi za Serikali na umma kwa ujumla”, amesema.
Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed salim (CFR) kinatoa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi za Astashahada ya awali, Stashahada, Stashahada ya Juu, Shahada na Shahada za Uzamili. Kwa upande wa kugha, Kituo kinatoa mafunzo ya lugha za kigeni zikiwemo Kireno, Kifaransa, Kichina, Kiarabu, kihispaniola na Kikorea. Aidha, mafunzo maalumu na kozi fupi katika masuala ya uongozi wa kimkakati, diplomasia na uhusiano wa kimataifa, stratejia, usuluhishi wa migogoro na ujenzi wa amani yameendelea kutolewa kwa wadau mbalimbali wakiwemo watumishi kutoka Taasisi za umma na Sekta binafsi.
