Habari
BALOZI KILIMA "UKANDA WA NCHI ZA MASHARIKI YA KATI NI UKANDA MUHIMU KATIKA SIASA ZA KIMATAIFA"

Balozi Abdallah Kilima, Mkurugenzi wa Idara ya masuala ya nchi za Mashariki ya Kati, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema Ukanda wa Nchi za Mashariki ya Kati ni Ukanda muhimu katika Siasa za Kimataifa.
Balozi Kilima amesema haya baada ya kutoa Mhadhara kwa Wanajumuiya, Wanataaluma na Wanafunzi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, kuhusu Siasa za Kimataifa “Geopolitics” kwa nchi za Mashariki ya Kati.
“Nimekuja kutoa Mhadhara katika Kituo chetu cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, kuhusu masuala ya Siasa za Kimataifa kwa nchi za Mashariki ya Kati na ndio eneo ambalo ninalifanyia na nimelifanyia kazi kwa muda mrefu na nina uelewa mkubwa kuhusu eneo hili, ambalo ni eneo muhimu kutokana na utajiri wa gesi na mafuta. Sisi kama Tanzania tunaiangalia Mashariki ya Kati kama eneo la Kimkakakti ambalo Tanzania inaweza kunufaika kutokana na fursa mbalimbali zinazopatikana. Fursa hizo ni pamoja na mikopo na misaada nafuu ambayo inapatikana kupitia Mfuko wa Kuwait “Kuwait Fund”, fursa nyingine zilizopo ni katika ajira, pamoja na kuuza bidhaa za chakula” amesema Balozi Kilima.
Balozi Kilima amesema kuwa kuna jitihada zinazoendelea katika ukanda huo za kutanua wigo wa shughuli zao za kiuchumi ili kupunguza utegemezi wa mafuta na rasilimali nyingine zinazotokana na nishati, ikiwa ni pamoja na kujihakikishia usalama wa chakula.
Akizungumzia kuhusu mashirikiano yaliyopo baina ya Tanzania na nchi za Mashariki ya Kati amesema kuwa ni katika nyanja za biashara na uwekezaji, mashirikiano ya kiuchumi na masuala ya kidiplomasia.