Habari
KUHITIMISHWA KWA KOZI YA UONGOZI NA UJUZI WA MAJADILIANO KATIKA KITUO CHA DKT. SALIM AHMED SALIM
Dar es Salaam, Washiriki wa kozi fupi ya Uongozi na Ujuzi wa Majadiliano katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim leo wamehitimu rasmi mafunzo hayo baada ya kupitia wiki ya kujifunza mbinu muhimu za kiuongozi na kiuweledi.
Kozi hiyo imetoa maarifa ya kina kuhusu uongozi bora, mawasiliano ya kimkakati, pamoja na ujuzi wa majadiliano unaohitajika katika kutatua changamoto katika mazingira ya taasisi na jamii. Washiriki walipata nafasi ya kushiriki mijadala, mazoezi ya vitendo, na tathmini zilizoandaliwa ili kuongeza uwezo wao wa kufanya maamuzi, kuongoza timu, na kusimamia mivutano au migogoro kwa njia yenye tija.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkurugeni wa taaluma wa Kituo hicho, Dkt.Anita Lugimbana alisisitiza umuhimu wa viongozi wa sasa na wa baadaye kujenga uwezo wa mawasiliano na majadiliano, akibainisha kuwa ujuzi huo ni nguzo muhimu katika kuleta mabadiliko chanya ndani ya taasisi za umma na binafsi.
Washiriki wamepongeza programu hiyo kwa kuwapa mtazamo mpana zaidi kuhusu namna ya kuongoza kwa ufanisi, kujenga ushirikiano, na kuendeleza mazungumzo ya kujenga Katika maeneo yao ya kazi. Wametaja kuwa mafunzo hayo yataboresha utendaji wao na kuchochea ushirikiano katika kuleta suluhisho endelevu kwa changamoto wanazokutana nazo.
Mafunzo hayo yamehitimishwa kwa kukabidhi vyeti kwa washiriki na wito kwao kuendelea kutumia ujuzi waliopata katika kukuza uongozi wenye maadili na majadiliano yenye kuleta matokeo chanya katika jamii.
