emblem

Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim

Habari

MAPITIO YA TATHMINI YA UTENDAJI KAZI WA KITUO CHA CFR YAMEKAMILIKA- MHE. BALOZI KOMBO (MB)


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) amesema mapitio ya tathmini ya utendaji kazi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) yamekamilika na utekelezaji wake natarajia kuanza hivi karibuni kupitia Baraza la Uongozi wa Kituo .

Mheshimiwa Balozi Kombo (Mb) amesema haya wakati akiwasilisha Bungeni hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026.

Katika hotuba yake, mheshimiwa Balozi Kombo (Mb) amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2024/2025 Kituo kimedahili jumla ya  wanafunzi  1,646 kati yao 149 ni ngazi ya astashahada ya awali, 131 astashahada, 120 stashahada, 840 stashahada ya juu, 251 shahada na 155 stashahada ya uzamili. Amesema Kituo kinatoa mafunzo ya lugha za kigeni saba (7) ambazo ni Kiarabu, Kifaransa, Kihispania, Kiingereza, Kichina, Kikorea na Kireno.

Mheshimiwa Waziri Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) amesema Kituo kinatoa mafunzo ya muda mfupi katika masuala ya diplomasia, uhusiano wa kimataifa, stratejia, usuluhishi wa migogoro na ujenzi wa amani. Katika kipindi hiki mafunzo ya muda mfupi yametolewa kwa washiriki 221 kutoka katika Taasisi za Umma na Sekta Binafsi.

Katika mwaka wa fedha 2024/2025 amesema, Kituo kimesaini Hati za Makubaliano (MoU) na Taasisi za nje ambazo ni:- Hati ya Makubaliano kati ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) na Chuo cha Kidiplomasia cha  Saud N. Al Sabah cha Taifa la Kuwait pamoja na Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Kituo cha CFR na Taasisi ya CMI Martti Ahtisaari Peace Foundation.

Mheshimiwa Waziri Kombo (Mb) amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Kituo kinatarajia kutekeleza majukumu yafuatayo: -

1. Kuendelea kutoa mafunzo ya uhusiano wa kimataifa na Diplomasia na lugha ya Kiswahili kwa wageni;
 2. Kuendelea kutafiti maeneo ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia;
3. Kuendelea kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia;
4. Kuendelea kuwajengea uwezo wa kitaaluma watumishi wa Kituo;
5. Kuendelea kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu kwa wadau mbalimbali ikiwemo Serikali na Taasisi zake; na
6.  Kuendelea kukitangaza Kituo kitaifa na Kimataifa.