emblem

Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim

Habari

USAJILI WA WANAFUNZI WAPYA WA MWAKA 2025/2026 UMEANZA RASMI


Mapema Novemba 17, 2025 Wazazi na watoto wao wakiwa na nyuso zenye matumaini ya kuelekea kukamilisha ndoto za watoto wao ,Pamoja wamejitokeza kwa wingi Katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kuanza kufanya usajili wa wanafunzi hao wapya kwa mwaka wa masomo 2025/2026.

Miongoni mwao alikuwepo Neema, msichana mwenye hamu kubwa ya kujifunza masuala ya diplomasia na mahusiano ya kimataifa. Alisimama kimya katika foleni ya kusogea katika usajili huku akitafakari na baadae alisema.

“Hatimaye safari yangu inaanza,” alisema“Nimekuwa nikitamani kusoma hapa. Natumaini nitapata maarifa, marafiki wapya, na mwelekeo wa maisha yangu ya baadaye.”

Wakati akisubiri zamu yake, alionekana mwenye hofu ndogo kuhusu changamoto mpya, lakini pia alihisi nguvu na ari mpya. “Natarajia kukutana na walimu bora, kujifunza mambo mapya kuhusu dunia, na kufungua milango ya fursa ambazo sijawahi kuzifikiria,” alisema Neema.

Zamu yake ilipofika, alisogea mbele, akaweka nyaraka zake mezani. Afisa usajili alimtazama kwa tabasamu na kusema:

“Karibu. Sasa wewe ni mwanafunzi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa rasmi.”

Maneno hayo yalimfanya Neema apumue kwa furaha,na baada ya kukamilisha usajili wake, alionekana akitembea kutoka kwenye chumba cha usajili akiwa amejaa matumaini,hii haikuwa tu siku ya usajili bali ilikuwa siku ya mwanzo wa maisha mapya, hatua ya kuelekea kuwa mtaalamu wa kimataifa anayetamaniwa duniani kote.

Hata hivyo usajili huo bado unaendelea kufanyika ,na utahitimishwa Novemba 21,2025 hivyo wananchi wanakaribishwa kuja kuendelea na usajili huo.