Habari
WATANZANIA WAASWA KUJIFUNZA LUGHA ZA KIGENI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) ametoa wito kwa Watanzania kujifunza lugha za kigeni na namna ya kuzungumza kwa umma.
Mheshimiwa Balozi Kombo (Mb) amesema haya wakati wa mahafali ya 27 ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) yaliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNCC), Dar es Salaam.
“Ili kuhakikisha Watanzania wanashindana katika kupata fursa za kazi Kimataifa msisitizo mkubwa uwe ni katika kujifunza lugha za kimataifa na namna ya kuongea kwa umma” amesema mheshimiwa Kombo.
Akizungumza kuhusu mabadiliko yanayotokea Duniani amesema ni muhimu kwa wataalam na wahitimu kujifunza namna ya kutoa ushindani katika masuala ya Diplomasia katika nyanja za Kimataifa.
Kuhusu kuifungua nchi, amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameifungua nchi kupitia filamu ya “Royal tour” ambayo imeitangaza Tanzania Kimataifa.
Mheshimiwa Waziri Kombo (Mb) ametoa wito kwa Uongozi wa Kituo cha CFR kuboresha programu zake ili ziendane na mahitaji ya sasa kwa Wizara zetu, Mashirika ya Kimataifa, Sekta Binafsi na zaidi iwe ni kutoa programu zenye ubora na kiwango, na sio kuangalia idadi ya wingi wa udahili wa wanafunzi.