Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, zamani kikijulikana kama Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Msumbiji na Tanzania kilibadilishwa jina na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 30 Septemba 2023. Kituo hiki kilianzishwa mwaka 1978 kupitia Mkataba wa Uwili kati ya Serikali za Jamhuri ya Msumbiji na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Majukumu ya Msingi ya Kituo hiki ni kutoa mafunzo, kufanya tafiti, pamoja na kutoa huduma za ushauri kwa wadau wa sekta ya umma na sekta binafsi. Nchini Tanzania Kituo hiki kina hadhi ya kidiplomasia, kupitia Sheria ya Kinga na Haki za Kidiplomasia na Kibalozi, SURA 356.
Kituo hutoa mafunzo mahsusi na yaliyobuniwa kulingana na mahitaji ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kituo pia huandaa watumishi wa umma wanaopangiwa kutekeleza majukumu kwenye Balozi na Misheni za Tanzania nje ya nchi.
Vilevile, Kituo hutoa mafunzo ya muda mfupi kwa taasisi za sekta binafsi na umma. Pia kinatoa program za muda mrefu kuanzia Ngazi ya NTA Level 5 hadi NTA level 9, ambazo zote zina ithibati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).