TANGA: TANZANIA imeeleza kuwa inaendelea kutumia Diplomasia ya Uchumi kufungua fursa za biashara, uwekezaji na masoko kupitia ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa, ikiwamo maeneo huru ya biashara barani Afrika.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi kutoka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR), Maryciana Mhagama, amesema Diplomasia ya Uchumi inalenga kuimarisha nafasi ya Tanzania kiuchumi kwa kutumia fursa zinazotokana na mahusiano ya kimataifa.
Amesema msisitizo umewekwa katika uwekezaji, ukuaji wa biashara, mikutano, utamaduni na utalii, huku Tanzania ikiendelea kuimarisha ushirikiano katika ngazi ya uwili, kikanda na kimataifa.
Mhagama ameyasema hayo katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Tanga, ambako CFR ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026.
“Kwa kuzingatia fursa zilizopo, Tanzania inaendeleza Diplomasia ya Uchumi katika Uhusiano wa Uwili, Kikanda na Kimataifa,” amesema.
Amesema CFR pia inaandaa vijana kuwa mahiri na wenye weledi kupitia mafunzo mbalimbali ya Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia, Utawala wa Kimkakati na Diplomasia ya Uchumi.
Aidha, amesema Kituo kitaendesha mafunzo ya Diplomasia, Itifaki na Ustaarabu kuanzia Agosti 24 hadi 28, 2026, jijini Dar es Salaam, akiwataka wadau wa sekta ya umma na binafsi kutumia fursa hiyo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alifungua rasmi Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ubunifu na kuhakikisha bunifu zinazozalishwa nchini zinatumika kutatua changamoto za jamii na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Profesa Mkenda alisema, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu, ikiwamo kuwaunganisha na taasisi pamoja na sekta binafsi ili bunifu zao zifikie hatua ya kuwa bidhaa na biashara.
Watumishi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) wa...
Mheshimiwa Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed, Balozi wa Comoro nchini Tanzania, le...
Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim ( CFR), kimetoa wito...
Mafunzo ya muda mfupi kuhusu Itifaki za Mashirika na Uhusiano wa Serikali (Corpo...
Balozi wa Jamhuri ya Cuba nchini Tanzania, Mheshimiwa Yordenis Despaigne Vera, l...